Muungano wa NASA ndio utakao nasua Kenya kutoka gizani.
Muungano huu unatarajia kung’oa serikali ya Jubilee kutoka mamlakani mwaka ujao.
Hili lilikuwa pendekezo la kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, na limeungwa mkono na vingozi kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Huu ni muungano ambao utaleta mabadiliko. NASA itanasua Kenya kutoka kwa ubadhirifu wa mali ya umma, mauaji ya kiholeholela, siasa ya matusi, maendeleo yanayoegemea upande mmoja, uongozi wa kifamilia, vita vya kikabila, propaganda potovu, upeanaji wa nadhifa kwa misingi ya kabila na mengineyo.
Kenya inastahili kuungana chini ya mwavuli huu wa NASA kama ilivyofanyika mwaka wa 2002.
Wakenya wamechoka na viongozi wanaojishughulisha na kujaza tumbo zao karai kutumia mali ya umma.
Masikio ya wananchi yanaumwa kwa kusikia matusi kutoka kwa wanasiasa siku nenda siku rudi.
Akina mama hawataki kuendelea kudunishwa na kupigwa na viongozi wenzao, huku vijana wakiapa kutokuwa ngazi ya wanasiasa matapeli.
Miradi gushi imesheheni majimboni na katika serikali ya kitaifa. Inatumika kama mbinu ya kupora nchi.
Aidha, kampeni zimefanywa kuwa swala muhimu sana kuliko shida za Wakenya walala hoi.
Kenya imechoka na NASA ndio suluhu tosha. Chini ya uongozi wa wazalendo kama Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Isaac Ruto, Gideon Moi na wengineo; Kenya itaponywa.