Uhaba wa maji katika ukanda wa Pwani umekuwa tatizo kubwa huku wakaazi wakilazimika kutembea mwendo mrefu kutafuta bidhaa hiyo muhimu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ni kinaya kikubwa kwa wakaazi kukosa bidhaa hiyo haswa ikizingatiwa kuwa eneo hili lina vyenzo vya maji kadhaa, vinavyotumika na kampuni ya kusambaza maji hapa Pwani kwa kiasi kikubwa.

Kaunti ya Taita Taveta ambayo ni mojawapo ya kaunti kubwa hapa Pwani, inajivunia uwepo wa kituo cha chemichemi za maji cha Mzima Springs, ila bado wakaazi wanatatizika kutokana na uhaba wa maji.

Tatizo lilo hilo limekuwa likishuhudiwa na wakazi wa kaunti ya Kwale, haswa kutoka maeneo ya Kinango, licha ya kaunti hiyo kuwa na kituo cha chemichemi za maji cha Maremare.

Hivi majuzi, wakaazi wa eneo hilo waliripotiwa kutembea zaidi ya kilomita kumi ili kusaka bidhaa hiyo muhimu.

Kaunti ya Kilifi pia ilikumbwa na changamoto ya uhaba wa maji licha ya kujivunia uwepo wa kituo cha maji cha Baricho, kinachotumiwa sana na kampuni ya kusambaza maji ya Kilifi.

Mwezi jana, Gavana wa Kaunti hiyo Amason Kingi alianzisha miradi mbalimbali ya kufikisha maji katika maeneo mbalimbali katika kaunti ndogo ya Ganze, huku lori tano za maji zikiagizwa kugawa maji mara nne kwa wiki.

Aidha, swala la ukosefu wa maji katika Kaunti ya Mombasa limekuwa likishuhudiwa kila uchao, haswa katika maeneo ya Kisauni na Barsheba, licha ya afisi za halmashauri ya kusambaza maji kuwa katika kaunti hii.

Swali ni je, ni nani atakayekabiliana na swala la ukosefu wa maji hapa Pwani ikizingatiwa kuwa kaunti za pwani zinauwezo wa kutoa maji ya kutosha kwa raia wake?