Usalama barabarani kwenye njia ya Waiyaki hasa kutoka maeneo ya stani ya Kinoo ni donda sugu. Kila jioni, wasafiri wengi pamoja na wanaotumia barabara wamepoteza maisha yao kutokana na uendeshaji mbaya na matumizi mabaya ya barabara.
Japo kuna daraja za kuvukia, sehemu hizi si salama Abadan katan! Vivukio vya chini ya barabara vimesheheni vibaka na wezi ambao huwahangaisha watu. Ukosefu wa usalama katika maeneo haya kumewafanya wengi kuchagua heri kutumia sehemu zisizo faa kuvukia.
Madereva wengi wa magari makubwa kama trela wanaendesha magari kwa kasi ambayo haidhibitiki pakitokea jambo la dharura linalo hitaji breki. Magari yanaposhindwa kuthibitiwa, mengi hukosa mwelekeo na kuyagonga magari, watu na majengo kandokando ya barabara. Hili ni jambo linalohitaji hatua ya dharura kuokoa maisha ya wakazi wa maeneo ya barabara.
Polisi pamoja na washikadau wa uchukuzi na mawasiliano wanafaa kuchukua hatua za dharura ili kuleta suluhu za kudumu. Vifo vingi vinaweza kupunguzwa kwenye barabara hii. Watoto wa shule ambazo zipo kwenye maeneo ya barabara wataendelea kupoteza maisha yao kwa madereva na magari yanayoendeshwa ovyo. sheria za usalama barabarani zifunzwe zaidi kwa watu ili kuthibiti ajali hizi.