Jaji mkuu nchini David Maraga katika hafla ya awali. Amewaonya mahakimu na majaji wafisadi kuwa chuma chao ki motoni. Picha/ nation.co.ke
Jaji mkuu nchini David Maraga amewaonya mahakimu na majaji wafisadi kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza katika hoteli moja mjini Mombasa wakati wa ufunguzi wa hafla iliyowaleta pamoja mahakimu 123, Maraga aliahidi kupambana na ufisadi katika idara ya mahakama, ili kuhakikisha idara hiyo inatoa huduma kwa njia ya huru na haki.“Nitahakikisha hakuna ufisadi unaoendelezwa katika idara ya mahakama kote nchini na atakayepatikana atafutwa kazi,” alisema Maraga.Maraga alisema kuwa wamejizatiti kukabiliana na swala la ufisadi linaloendelezwa na baadihi ya maafisa wakuu mahakamani, hasa katika kesi zinazohusu ulanguzi wa mihadarati.Alisema kuwa kuna baadhi ya maafisa katika mahakama za humu nchini wanao shirikiana na walanguzi wa mihadarati, na kuongeza kuwa tayari wameweka mikakati ya kuwanasa maafisa hao.Kauli hii inajiri siku chache baada ya katibu mtendaji katika Baraza la maimamu na wahubiri CIPK, Sheikh Mohamed Khalifa kuishutumu idara ya mahakama kwa madai ya kulemaza vita dhidi ya mihadarati.Maraga aidha amesema kuwa idara hiyo itahakikisha kila Mkenya anapata haki na usawa akiwa mahakamani.“Kila mkenya atahudumiwa kwa usawa kote nchini, hakuna kubaguliwa,” alisema Maraga.