Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari anatarajiwa kuzuru nchini Januari 27.
Ziara hiyo inalenga kuboresha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili.
Akihutubia wanahabari siku ya Jumatano katika ikulu ya Mombasa, msemaji wa ikulu ya rais Manoah Esipisu amesema viongozi wa mataifa haya mawili watafanya mazungumzo ya kina kuhusu uboreshaji wa biashara ikiwemo sekta ya kilimo.
Esipisu ameeleza kuwa ziara ya rais katika eneo la Pwani imemulika zaidi utekelezaji wa ahadi za serikali yake ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2013. Alitaja uboreshaji wa bandari, ujenzi wa reli na viwanja vya ndege miongoni mwa miundo mbinu eneo hilo.
Wakati huo huo amesema mapema mwezi Februari, rais wa Misri Abdel Fattah Al-sisi anatarajiwa kuzuru Kenya.
Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kwa rais wa Misri aliye madarakani kuzuru Kenya.
Aidha rais Uhuru Kenyatta ataondoka humu nchini Januari 30 kuelekea jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo suala la mzozo nchini Burundi litajadiliwa.