Serikali ya Marekani ikishirikiana na shirika moja la kijamii mjini Mombasa imefungua maktaba ya kisasa mjni humo, kama njia moja ya kuimarisha viwango cha elimu.
Maktaba hiyo iliyopewa jina la Ali Mazrui Memorial Liblary kumhenzi msomi maarafu duniani na ambaye ni mzaliwa wa mjini humo Profesa Ali Mazrui, ilizinduliwa rasmi katika mtaa wa majengo siku ya Jumanne.
Balozi wa Marekani nchini Kenya ambaye ndiye aliyeongoza uzinduzi huo Robert Gordec alisema kwamba Marekani imejizatiti kubadilisha viwango vya elimu barani Afrika.
Alisema Mombasa imebahatika kufaidika na mpango huo wa maktaba ya kisasa chini ya mpango wa American Corner.
“Tutaleta tarakilishi pamoja na vitabu ambavyo vitasaidia wanafunzi kusoma mambo mengi yanayohusu nchi yao pamoja na dunia kwa ujumla.” alisema Gordec.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alipongeza mpango huo na kuahidi kwamba serikali yake itasaidia kununua vitabu pamoja na kusaidia katika upanuzi wa jengo hilo.
“Miaka kadhaa iliyopita mtaa huu wa Majengo ulijulikana kwa sifa mbaya ya vijana kuingilia mambo ya uhalifu. Mpango huu wa maktaba eneo hili ni ishara kwamba kuna mabadiliko na elimu itasaidia kubadilisha zaidi sehemu hii,” alisema Joho.
Hapo awali, mtaa huo wa Majengo mjini Mombasa uligonga vyombo vya habari kufuatia vijana kuhusishwa na makundi ya itikadi kali za kidini, huku polisi wakikabiliana nao mara kwa mara.
Mpango huo wa kuzindua maktaba hiyo umepokelewa vyema na wakaazi, wengi wao wakisema utasaidia watoto kukua na madili mema pamoja na kujifunza teknolojia mbalimbali.