Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa maswala ya ndani wa Marekani Bi Sally Jewell pamoja na waziri wa mazingira humu nchini Bi Judy Wakhungu walizuru Bandari ya Mombasa siku ya Jumanne kufanya ukaguzi maalum bandarini humo.

Ziara hiyo inakuja siku moja baada ya mataifa haya mawili kutia saini makubaliano ya pamoja ya kuimarisha vita dhidi ya uwindaji haramu na usafirishaji wa bidhaa haramu kupitia bandari za humu nchini.

Akiongea bandarini humo, Jewell alisema kwamba mkataba huo utahakikisha kwamba Marekani inashirikiana vilivyo na Kenya kulinda mbuga za humu nchini.

“Nafahamu kwamba bandari hii imekuwa ikitumika vibaya katika biashara haramu. Hata hivyo, sasa tumekubaliana kwa pamoja kwamba tutaimarisha shughuli za kufuatilia biashara zinavyoendeshwa bandarini,” alisema Bi Jewell.

Aidha, waziri huyo anayeshikilia wizara muhimu katika taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani, alisifu Kenya kwa juhudi izake katika vita vya kukabili biashara ya kuingiza bidhaa za magendo.

Kwa upande wake, waziri wa mazingira nchini Bi Judy Wakhungu alisema kuwa utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kwamba taifa hili la Kenya limepiga hatua kubwa katika vita hivyo.

“Wafanyibiashara haramu wamekuwa wakitumia bandari hii ya Mombasa kutokana na kwamba ni kubwa na pia inaendesha shughuli nyingi kwa pamoja. Lakini sasa kupitia ushirikiano na nchi ya Marekani, haya yote yatakwisha,” alisema Wakhungu.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Balozi wa Marekani humu nchini Robert Godec, mkurugenzi mkuu wa KPA Gichiri Ndua, pamoja na maafisa wengine wakuu serikalini.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta aliongoza zoezi la kuharibu bidhaa ghushi zilizopatikana bandarini Mombasa, ikiwa ni pamoja na sukari na mchele.

Rais Kenyatta alitangaza kwamba serikali itaendelea kupiga vita biashara hiyo ambayo imekuwa ikiendeshwa bandarini humo kisiri.