Serikali ya Marekani imesema kuwa imetoa vifaa maalum kwa taifa la Kenya vitakavyotumika na maafisa wa usalama, pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa maafisa wanaohudumu katika Bandari ya Mombasa, ili kuimarisha shughuli za usalama katika sehemu hiyo.
Haya yamejiri wakati wa ziara ya waziri wa usalama wa Marekani Bi Sally Jewell bandarini humo siku ya Jumanne, kufanya ukaguzi katika sehemu za kuingiza pamoja na kutoa mizigo.
Vifaa hivyo vitatumika katika kufanyia watu na mizigo inayoingia au kutoka bandarini ukaguzi ili kukabili biashara yotote haramu itakayonuiwa kufanyika sehemu hiyo.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho ameipongeza ziara ya waziri huyo wa Marekani akisema kwamba itaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi baina ya mataifa yote mawili.
Katika taarifa aliyoweka katika mtandao wake wa kijamii siku ya Jumanne baada ya kuhudhuria hafla ya kumkaribisha waziri huyo, Joho alishukuru Marekani kwa kutoa vifaa hivyo.
“Kwa niaba ya kaunti ya Mombasa ningependa kutoa shukrani zangu kwa taifa la Marekani kwa moyo walioonyesha kusaidia kuimarisha usalama katika Bandari yetu. Ni ishara kwamba tatizo la kuingizwa kwa bidhaa haramu hapa nchini litakwisha,” alisema Joho.
Ziara hiyo pia imegusia zaidi usafirishaji wa dawa za kulevya unaoaminika kufanyika kupitia bandarini, huku Gavana Joho akisema kuwa walifanya mazungumzo ya kina kutafuta suluhu kwa swala hilo.
Ushirikiano baina ya Marekani na Kenya katika vita hivyo unatarajiwa kusaidia kugundua kwa mapema bidhaa zisizo halali zinazopitishwa eneo hilo.
Waziri huyo wa Marekani pamoja na mwenzake wa Kenya Bi Judy Wakhungu waliweka saini ya makubaliano katika ofisi kuu ya huduma za wanyamapori KWS mjini Nairobi siku ya Jumatatu siku moja kabla ziara ya Mombasa.