Share news tips with us here at Hivisasa

Huku uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 ukikaribia, wanasiasa wamo mbioni kushawishi wapiga kura katika eneo la Gusii ambapo wikendi hii imepita imeshuhudia wanasiasa waliwarai jamii ya wakisii kujisajili kupiga kura.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la 10 Kenneth Marende aliwaomba jamii ya Wakisii kujiandikisha kwa wingi kwa kujiandikisha kama wapiga kura ili angalau jamii kutoka maeneo ya Magharibi mwa Kenya kupata Rais mwaka wa 2017.

Marende alikuwa akiongea katika Kanisa la SDA la Nyosia lililoko eneo Bunge la Nyaribari Chache, siku ya Jumamosi, walipokuwa katika hafla ya kuchangisha pesa kwa kanisa hilo ambapo aliwataka Wakisii wote kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

"Wakisii na Waluhya ni kitu kimoja tangu zamani na tungependa umoja huo kuendelea zaidi, hivyo nawasihi muwe karibu na vituo vya kujiandikisha pindi usajili wa wapiga kura utaanza hivi karibuni ili tuamue nani anafaa katika urais mwaka wa 2017,’ alihoji Marende.

Spika huyo wa zamani alikuwa ameandamana na Mbunge wa eneo hilo Richard Tong’i, Mwenyekiti wa CIC Charles Nyachae, Mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo pamoja na viongozi wengine wa Kaunti ya Kisii ambao wote kwa pamoja waliwaomba wakazi wa Kisii kuiombea nchi ili tuwe na amani.