Mshirikishi mkuu wa eneo la Pwani Nelson Marwa ameahidi kuwatia mbaroni walanguzi wakuu wa dawa za kulevya.
Marwa amewataka maafisa wa polisi kufanya msako mkali dhidi ya walunguzi hao, wanaosemekana kuendeleza biashara yao katika eneo la Pwani.
Ameongeza kuwa dawa nyingi za kulevya zinaingizwa humu nchini kupitia maeneo tofauti ya mipaka ya Pwani.
“Mihadharati inaingizwa kupitia mipaka yetu, hivyo sharti usalama uimarishwe na wahusika kutiwa mbaroni,” alisema Marwa.
Marwa ametaja kaunti za Lamu, Kilifi, Mombasa na Kwale kama maeneo sugu ambayo yanatumiwa kuingiza dawa za kulevya nchini.
“Haya maeneo ndio hutumiwa kupitisha dawa za kulevya eneo la Pwani,” alisema Marwa.
Aidha, amesema Bandari ya Mombasa inakiuka kanuni za kuthibiti uingizaji wa mihadarati nchini, huku akiilaumu halmashauri ya bandari kwa kushindwa kusajili boti za usafiri.
Marwa amemtaka kamanda wa polisi katika ukanda wa Pwani James Akoru kuanzisha msako katika Bandari ya Mombasa kuanzia siku ya Jumatatu, juma lijalo.