Idara ya usalama Pwani imeahidi kuimarisha usalama katika kila pembe ya eneo hilo ili kuhakikisha kuwa wakaazi wanaishi kwa amani, hasa wakati huu ambapo taifa linakaribia kufanya uchaguzi mkuu.
Mshirikishi mkuu wa utawala katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa, amesema kwamba madai ya kuwa Kaunti ya Tana River inakabiliwa na ukosefu wa usalama ni uvumi tu wa baadhi ya watu fulani wanaolenga kuzigonganisha jamii zinazoishi katika eneo hilo ili kushuhudiwe machafuko.
Akizungumza na wanahabri mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Marwa alisema kuwa atakayepatikana akijaribu kuwachochea wakaazi wa Tana River kuzua vita vya kikabila atakabiliwa kwa mujibu wa sheria kwani usalama wa wananchi ni muhimu nchini.
Aidha, alisema kuwa serikali imebaini njama inayopangwa na baadhi ya viongozi fulani ili kuvuruga usalama wa eneo hilo na kujipatia umaarufu wa kisiasa wakati wa uchaguzi.
"Serikali iko macho na tumebaini kuwa kuna baadhi ya watu fulani wanaowagonganisha wakaazi wa Tana River kwa nia ya kuvuruga usalama wa eneo hilo ili wapate umaarufu wa kisiasa. Sisi hatutakubaliana na hayo na lazima watu hao wakabiliwe,” alisema Marwa.