Mshirikishi mkuu wa utawala katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa amefutilia mbali madai ya baadhi ya wawakilishi wadi katika Kaunti ya Mombasa kuwa alichochea ubomoaji wa nyumba za watu katika Uwanja wa Ndege wa Moi jijini Mombasa bila kuhusisha serikali ya kaunti.
Wawakilishi hao wakiongozwa na Ibrahim Abdallah, mwakilishi wa Wadi ya Kipevu, walitoa lalama hizo katika Bunge la Kaunti ya Mombasa siku ya Jumanne wakimtaka Marwa kukoma kujihusisha na masuala yasiyomhusu.
Marwa hata hivyo akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, wakati wa kuzinduliwa kwa kaunti ndogo ya Nyali, alisema kuwa wajibu wake ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata usalama wa kutosha.
Aidha, alipinga madai kuwa anawasilisha malengo yake binafsi kando na ya wananchi.
“Madai haya ni siasa tu zinazoenezwa na wawakilishi hawa. Kazi yangu ni kulinda usalama wa kila mwananchi Mombasa na iwapo kunatokea hofu wowote wa usalama, sina budi kuingilia kati na kutahadharisha watu,” Marwa alielezea.
Wawakilishi wadi hao pia wamewaomba wananchi katika eneo hilo la Uwanja wa Moi kususia mpango huo wa ubomoaji na kuwaondoa katika sehemu hiyo hadi pale swala hilo litakapowekwa wazi na gavana Hassan Joho pamoja na viongozi wengine wakuu katika kaunti hiyo.