Afisi ya mbunge wa Mvita imelaani hatua ya serikali kupiga marufuku mradi wa utoaji chakula kwa wanafunzi wa darasa la nane, wanaofanya mtihani wa kimataifa wa KCPE.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubia wanahabari kwenye shule ya chekechea ya Mbaraki jijini Mombasa, mwenyekiti wa hazina ya ustawishaji wa eneo bunge la Mvita Omar Shariff, amesema kamwe hawana uhusiano wowote na wizi wa mitihani.

“Hatujawahi husika na wizi wa mitihani kwa kuwa kazi yetu ni kutoa chakula kwa wanafunzi pekee,” alisema Shariff.

Alisema kuwa afisi hiyo haijawahi husika katika visa vya wizi wa mitihani, katika kipindi cha miaka saba tangu kuanza kwa mradi huo wa ugavi wa chakula kwa watahiniwa.

Shariff aliitaja hatua hiyo kama yenye mkono wa kisiasa na kumtaka mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa, kutoingiza siasa kwenye miradi ya manufaa kwa wananchi.

“Tuache kuingiza siasa kwenye miradi ya kusaidia wananchi,” alisema Shariff.

Aliongeza kuwa hatua hiyo haitaathiri afisi ya mbunge bali itawaathiri wanafunzi ambao hawana chakula wakati huu wanaposhiriki mtihani wao wa mwisho kwenye shule za msingi.

Sharrif alisema kuwa watapeleka vyakula hivyo kwenye nyumba za mayatima pamoja na madrasa ili kuepuka kuharibika kwa vyakula hivyo ambavyo vimewagharimu shilingi milioni 2.4.

Kauli hii inajiri baada ya mratibu mkuu wa ukanda wa Pwani, Nelson Marwa kupiga marufuku ugavi wa chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na upili katika Kaunti ya Mombasa.