Mshirikishi mkuu wa usalama katika kanda ya Pwani Nelson Marwa ameikashifu serikali ya Kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Hassan Joho kwa kushindwa kujadili miswada ambayo itakabiliana na biashara ya mihadarati katika kaunti hiyo.
Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Marwa alilitaka bunge hilo la kaunti kujadili miswada yenye manufaa kwa wakaazi.
“Badala ya bunge la kaunti kujadili miswada ya maana, kila mara wao hujadili miswada yanayomhusu Marwa,” alisema Marwa.
Hata hivyo, Marwa alisema kuwa ataendelea kukabiliana vikali na watu wanaouza mihadarati katika kaunti hiyo.
Alisema kuwa ni muhimu kukabiliana na biashara hiyo kwa kuwa utumizi wa mihadarati ndio chanzo kikuu cha kuchipuka kwa makundi ya uhalifu katika kaunti hiyo.