Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Photo/ the-star.co.ke]

Share news tips with us here at Hivisasa

Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa amemsimamisha kazi chifu wa eneo la Hindi, Kaunti ya Lamu.Haya yanajiri baada ya watu wanne kutoka kijiji hicho kuuawa na washukiwa wa kundi la al-Shabaab siku ya Jumatano.Akizungumza kwenye mkutano wa kiusalama huko Hindi siku ya Ijumaa, Marwa alisema kuwa chifu Hamisi Keya atasimamishwa kazi mpaka pale uchaguzi katika mauaji hayo utakapokamilika.Naibu chifu Abdalla Lausi atashikilia nafasi hiyo kwa sasa.Marwa alimkosoa chifu huyo kwa kushindwa kufanya kazi yake kikamilifu, hali aliyosema imechangia kushuhudiwa kwa ongezeko la mashambulizi ya kigaidi.Marwa alichukua hatua hiyo baada ya mkuu wa oparesheni ya Linda Boni Joseph Kanyiri kupendekeza maafisa wa usalama waliozembea kazini katika Kaunti ya Lamu kupigwa kalamu.Kanyiri alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wakaazi wa Lamu wakiendelea kuuawa na magaidi ilhali kuna maafisa wa usalama katika eneo hilo.Kanyiri aliwakosoa maafisa hao kwa kukosa kufika haraka katika tukio la siku ya Jumatano ambapo watu wanne waliuawa katika eneo la Hindi.“Maafisa wa usalama walishindwa kufika kwa muda unaofaa, hali iliyofanya watu wanne kuuawa kinyama,” alisema Kanyiri.Kauli yake iliungwa mkono na kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Lamu Muchangi Kioi aliyewahakikishia wakaazi kuwa usalama utaimarishwa.