Share news tips with us here at Hivisasa

Mshirikishi wa usalama katika kanda ya Pwani Nelson Marwa amemtaka  kamanda mkuu wa maafisa wa polisi wa utawala Mohammed Jira kuhamia katika eneo la Kisauni, kufuatia usalama katika eneo hilo kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza katika mkutano na washikadau wa usalama mjini Mombasa siku ya Jumanne, Marwa alisema kuwa Jira anastahili kukaa katika eneo la Kisauni ili kuhakikisha kuwa hakuna vurugu yoyote pamoja na kuthibiti hali ya usalama ya wakaazi.

Amri ya kiongozi huyo inajiri wakati ambapo eneo bunge la Kisauni limekua likikabiliwa na changamoto ya usalama, baada ya vijana wenye umri wa miaka kati ya 15-18, kuvamia wananchi na mapanga huku wakiwaibia mali yenye thamani.

Marwa alisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote ambaye atapatikana akifadhili vijana hao kwa njia yoyote.

Aidha, alitoa onyo kali kwa vijana ambao wamekuwa na tabia ya kungoa taa za serikali ambazo zimewekwa kwa ajili ya usalama hasa masaa ya usiku.

Kumekuwa kukishuhudiwa visa ambapo baadhi ya vijana hupanda katika milingoti ya taa za umma na kuiba bidhaa hizo ili kuwawezesha wahalifu kutekeleza uwizi wakati wa usiku.