Mshirikishi mkuu wa usalama kanda ya Pwani Nelson Marwa amesisitiza kuwa hakuna visa vyovyote vya wizi wa mitihani ya kitaifa vitakavyoshuhudiwa katika eneo la Pwani mwaka huu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari afisini mwake, Marwa alisema serikali imeweka mikakati dhabiti ya kukabiliana na wizi wa mitihani hiyo.

Alisema kuwa serikali imeweka makasha katika kila eneo bunge hapa Pwani, ambayo yatatumika kuhifadhi mitihani pindi itakapowasili kutoka Nairobi.

Aliongeza kuwa makasha hayo yatakuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Marwa aidha alisema kuwa wataanzisha uchunguzi wa hali ya juu kwenye shule zilizoko Mombasa, ambazo wamepokea ripoti za kuhusika katika wizi wa mitihani.

“Serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha hakuna mitihani inayoibiwa kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Hakuna mtu ataruhusiwa kuzunguka karibu na mazingira ya shule,” alisema Marwa.

Amewataka wazazi na wanafunzi kuwa makini na matapeli wanaotunga mitihani yao kwa ajili ya kuendeleza biashara haramu, na kupiga ripoti mara moja wanaposhuhudia visa kama hivyo.

Wakati huo huo, amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia wanafunzi kadi za heri njema zenye picha zao.