Mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa, ameitaka idara ya polisi kutohangaisha jamii za Wachonyi na Wakauma.
Akiwahutubia wakaazi katika eneo la Ngamani, Marwa alisema kuwa jamii hizo mbili zimekua zikihangaishwa kwa madai ya kuhusika na vuguvugu la MRC.
Alisema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu, kwani wanachama wote wa jamii hizo sio wahalifu.
Hata hivyo, amewataka polisi kuwasaka wanachama wa MRC ili waweze kukabiliwa kisheria.
“Tafuteni wahalifu wa MRC na muache kuhangaisha wakaazi wasiokuwa na hatia,” alisema Marwa.
Kauli hii inajiri baada ya jamii hizo mbili kulalamikia kuhangaishwa na maafisa wa polisi wanaowahusisha na kundi la MRC.
Kundi la MRC linadaiwa kutatiza shughuli za kiserikali kama vile usajili wa kura na vitambulisho vya kitaifa, na pia kutatiza uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 kwa kuvamia kituo cha kuhesabia kura cha Chumani katika Kaunti ya Kilifi.
Hata hivyo, viongozi wa kundi hilo wamepinga madai hayo ya kuhusishwa na uhalifu.