Wananchi wameonywa dhidi ya kutuma jumbe za uhalifu kwa mitandao ya kijamii ambazo hazijathibitishwa na idara ya usalama jijini Mombasa.
Akitoa onyo hilo siku ya Jumanne kwenye kikao na wanahabari afini mwake, Kamishana wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kuwa hali hiyo inakiuka maadili ya idara ya uslama kwani hatua zozote za uvamizi ama ukosefu wa kiusalama hazitolewi hadharani kabla ya kuthibitishwa na wakuu wa usalama.
Marwa aliwataka wananchi wanaomiliki vikundi katika mitandao ya kijamii kushirikisha polisi kwanza kabla ya kuchapisha jumbe hizo mitandaoni.
Aidha, aliongeza kuwa hatua hii ya kuweka jumbe hizo kiholela zinazua hofu za kiusalama miongoni mwa jamii ikizingatiwa hasa nyingine si za ukweli.
Vile vile, aliongeza kuwa huenda vikundi hivi vikatatiza usalama wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017.
Kauli yake iliungwa mkono na Kamanda Mkuu wa Polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi.
Kauli hii inajiri baada ya kushudiwa vikundi vingi kwenye mitandao ya kijamii kama vile 'Crime Alert', ambavyo vinatatiza shughuli za idara ya usalama hasa kazi ya maafisa wa upelelezi .
Itakumbukwa wiki chache zilizopita, Marwa aliagiza kufungwa kwa kikundi cha 'Crime Alert' kinachokisiwa kuingilia shughuli za idara ya usalama jijini, jambo lililopingwa na Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho.