Mshirikishi wa kanda ya pwani Nelson Marwa amewalaumu wawakilishi wa wadi Mombasa kwa kuwapotosha wananchi kuhusu kuhamishwa watu wanaoishi karibu na uwanja wa ndege wa Moi.
Marwa amewataja wawakilishi hao kama viongozi wasiofikiria kwa kina kabla ya kupinga mambo.
Aidha Marwa alieleza sababu ya kuwaondoa watu hao eneo hilo akisema ni kutokana na sababu za kiusalama kwa uwanja huo.
Alisema kuwa wafanyibiashara hasa wa kutengeza magari wamekuwa wakiendesha shughuli zao hadi karibu na uwanja huo jambo linalohatarisha usalama.
Akiongea katika eneo la Mkomani huko Nyali siku ya Jumanne, Marwa alisema wafanyibiashara hao wanafaa kutoka eneo hilo ili kuhakikisha kuwa magaidi hawawezi kuichukua nafasi hiyo kutekelza uhalifu.
“Watu wameweka vituo vya kutengeza magari mpaka karibu kabisa na uwanja huo, kwanini wasitafutiwe sehemu nyingine ya kufanyia biashara kwani lazima eneo hilo tu.” Alisema Marwa.
Wakati huo huo Marwa aliongeza kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi uko katika hali mbaya ikilinganishwa na hali halisi ya viwanja vya ndege kutokana na kuzungukwa na nyumba nyingi za makaazi eneo hilo.
“Ukienda katika viwanja vingine vya ndege utaona tofauti kubwa sana, ni ahibu ukiona kiwanja kama hiki tena cha kimataifa kikiwa kimezengukwa na nyumba kila mahali, tunataka tuweke viwango vinavyofaa.” Aliongeza Marwa.
Mapema siku ya Jumanne wawakilishi katika bunge la kaunti walifanya mkutano kupinga hatua hiyo wakisema ni kinyume cha sheria.