Idara ya usalama ukanda wa Pwani imelitaja eneo la Kisauni kama maficho ya wahalifu sugu, hasa washukiwa wa ugaidi.
Hii ni baada ya visa kadhaa vya uhalifu kuripotiwa katika eneo hilo, ikiwemo kuuawa kwa washukiwa wakuu wa ugaidi.
Mshirikishi mkuu wa eneo la Pwani Nelson Marwa amesema tukio la mshukiwa wa ugaidi na wizi wa mabavu Ismail Shosi kuuawa huko Kisauni siku ya Jumanne, linaashiria huenda kukawa na mtandao mkubwa wa wahalifu hasa washukiwa wa ugaidi katika eneo hilo.
Mnamo Julai 21, mwaka huu, washukiwa wawili wa ugaidi waliokuwa wakisakwa na polisi waliuawa katika nyumba ya mmoja wao katika eneo la Junda-Mishomoroni, Kisauni.
Marwa kwa muda mrefu amekuwa akilaumu uongozi wa eneo bunge hilo kwa kutojitokeza kukashifu ongezeko la visa vya uhalifu katika eneo hilo.
“Kwanini Kisauni kila mara na hatusikii viongozi wakikemea mambo kama haya?” aliuliza Marwa.
Aidha, Marwa amewataka viongozi wa eneo hilo kushirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha wanapiga vita uhalifu ili eneo la Pwani kuwa salama.