Mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa ametishia kulipua msitu wa Boni ili kuangamiza kundi la Al-Shabaab linalodaiwa kujificha kwenye msitu huo huko Lamu.
Marwa amesema kuwa kundi hilo limegeuza msitu huo kuwa kambi yao kuu ya maficho na mafunzo ya kivita.“Wanatumia msitu wa Boni kama maficho yao makubwa. Hatutakubali hilo kabisa na tutalipua msitu huo mara moja,” alisema Marwa.Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Mtongwe, Marwa alisema kuwa hivi karibuni kutasikika milipuko ambayo itatekelezwa na maafisa wa Kenya katika msitu huo na kuwataka wananchi wa eneo hilo kutoshtuka wanaposikia milpuko hiyo.“Kutakuwa na milipuko na milio ya risasi katika msitu huo, musishtuke kabisa,” alisema Marwa.Aidha, amewataka wananchi wanaoishi karibu na msitu huo kushirikiana na polisi katika kuripoti na kuangamiza magaidi.“Toeni ripoti kwa polisi iwapo mutashuku mienendo ya magaidi katika msitu huo,” alisema Marwa.Aidha, Marwa alisema kuwa ataongoza oparesheni hiyo yeye mwenyewe ili kuwapa maafisa wa usalama motisha.“Nitakuwa mstari wa mbele kuongoza oparesheni hiyo ya kuangamiza magaidi katika msitu wa Boni,” alisema Marwa.Siku ya Jumanne, maafisa wanne wa polisi na wanafunzi wanne waliuawa baada ya gari gari lao kukanyaga kilipuzi huko Lamu.