Idara ya usalama katika kaunti ya Mombasa imeahidi kuweka usalama dhabati katika kila eneo wakati wa ziara yake Baba Mtakatifu Papa Francis wa kwanza atakapozuru humu nchini.
Kwenye mkao na wanahabari katika makao makuu ya idara hiyo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alisema kwamba waumini wa dini ya kikristu wanaopanga kwenda jijini Nairobi kuhudhuria ibada takatifu itakayoungozwa na baba mtakatifu watapewa ulinzi wa kutosha.
Marwa amesema kwamba tayari idara hiyo imepokea idadi ya watu watakaosafari kuelekea jijini Nairobi pamoja na idadi ya magari ya uchukuzi wa umma, na akasema kwamba usalama utaimarishwa kwa waumini hao hadi jijini Nairobi.
Kamishna Marwa amewaonya vikali wanaolenga kuvuruga usafiri huo kukoma mara moja kwani maafisa wa usalama watakua macho.
"Tungependa kutoa onyo kali kwa wale wanatadhani kwamba maafisa wa polisi wamelala, wachunge sana tutawakabili kikamilifu iwapo watajaribu kuvuruga msafara wa waumini kwani wanyewe wanaenda kuhudhuria ibada maalum ya baba mtakatifu. Tutawapatia ulinzi wa kutosha na wataandamana na maafisa wa wa usalama," alisema Marwa.
Kamishna huyo wa kaunti amezidi kuwahakikishia wakazi wa kaunti ya Mombasa usalama dhabiti, huku akiwahimiza kushirikiana na maafisa wa polisi na kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu na kutiwa nguvuni.