Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Picha/ the-star.co.ke]
Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa amewaonya wanasiasa wanaowafadhili wanamgambo wa al-Shabaab katika Kaunti ya Lamu.Akiwahutubia wanahabari huko Lamu siku ya Ijumaa, Marwa alisema maafisa wa usalama wamepokea taarifa kuwa baadhi ya wanasiasa wanafadhili magenge ya ugaidi ambayo yamekuwa yakiwashambulia wakaazi na kuwaua.“Tumepokea taarifa kuhusu wanasiasa hao na tayari tumeanza uchunguzi. Mkono wa sheria utawakabili vilivyo hivi karibuni,” alisema Marwa.Hatahivyo, Marwa alidinda kutaja majina ya wanasiasa hao hadharani.“Hatutataja majina yao kwa sasa ila chuma chao ki motoni,” alisema Marwa.Wakati huo huo, Marwa amewataka wakaazi kushirikiana na idara ya usalama katika kukabiliana na visa vya ugaidi eneo la Lamu.“Tunawaomba mushirikiane na polisi kwa kutoa habari kuhusu magaidi ili usalama uimarike zaidi,” aliongeza Marwa.Kauli yake inajiri baada ya visa vya mashambulizi yanayotekelzwa na washukiwa wa kundi la al-Shabaab kuongezeka katika Kaunti ya Lamu.Siku ya Jumatano, watu wanne waliuawa baada ya wanamgambo hao kushambulia kijiji cha Hindi.