Mshirikishi mkuu wa usalama katika kanda ya Pwani Nelson Marwa amewataka wazazi na wakaazi kwa jumla kushirikiana na serikali ili kukabili janga la utumizi wa mihadarati katika eneo hilo.
Akizungumza katika afisi yake na wanahabari siku ya Jumamosi, Marwa alisema kuwa serikali ipo imara katika vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati eneo la Pwani, huku akiyataka mashirika ya kijamii kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa zozote zinazohusiana na ulanguzi wa mihadarati nchini kote.
Marwa alisema kuwa walanguzi wa mihadarati wameharibu maisha ya vijana wengi katika eneo la Pwani, na kuwafanya kuishia kuwa waathiriwa wa dawa za kulevya, jambo ambalo alisema limepelekea kuwa na utovu wa usalama katika maeneo mengi ya Pwani.
Aidha, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona vijana wengi walio na taswira ya mafanikio katika maisha yao kuanza kutumia dawa za kulevya.
Alisema kuwa dawa hizo zinawafanya kupoteza fahamu na kuishia kuwa wasio na manufaa kwa kuzurura ovyoovyo kwenye makazi ya wenyewe mwishowe kuanza kuwa wezi ili kukidhi mahitaji yao.
Marwa aliwasihi viongozi wa kisiasa kuingilia kati ili kuhakikisha kuwa idadi ya vijana wanaotumia mihadarati inapungua kwa kuwa huenda eneo la Pwani likawa linapoteza vijana muhimu sana katika uongozi wa baadae.
Haya yanajiri baada ya kukamatwa kwa jamaa mmoja huko mariakani akiwa na takribani kilo mia nne za bangi.