Idara ya usalama kaunti ya Mombasa imeshikilia kutolegeza kamba kupigana vita walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya hadi pale biashara hiyo haramu itakapositishwa.
Kulingana na kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, tayari maafisa wa polisi, viongozi wa kisiasa, wale wakidini na mashirika ya kijamii wanashirikiana kuona mihadarati inaangamizwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Marwa amesema kwamba atakayepatikana akiwashawishi vijana kutumia mihadarati wala kuuza dawa hizo atakabiliwa kikamilifu na maafisa wa polisi kwani hatua hiyo imedidimiza ndoto ya vijana wengi.
“Tunawaomba walanguzi wote wa mihadarati kuwacha kufanya biashara hio haramu na kujihusisha na maswla mengine ya kimaendeleo la sivyo mkono wa sheria utawaandama,” alisema Marwa.
Marwa, amewahimiza wakazi kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari kuhusu walanguzi na watumizi wa mihadarati ili kutiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka pamoja na kuwanasuru vijana wadogo waliyoathiriwa na dawa hizo.
“Tunawaomba wakaazi kujitokeza na kushirikiana na maafisa wa polisi katika kutoa habari kuhusu washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati ili watiwe nguvuni na kufunguliwa mashtaka,” aliongeza Marwa.
Operesheni hiyo ya kuwasaka walanguzi na watumizi wa dawa za kelevya imechangia pakubwa kujiwasilisha kwa vijana waliyoathirika kwa maafisa wa polisi ili kusaidiwa kupelekwa katika vituo vya kurekebishia tabia waraibu.
Kufikia sasa, zaidi ya waathiriwa mihadarati 100 wamejiwasilisha kwa maafisa wa polisi na kupelekwa katika vituo vya kurekebishia tabia.