Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya usalama Mombasa imesema maafisa wa usalama watakaopatika wakibugia pombe ama wakiwa walevi watafutwa kazi.

Akitoa onyo hilo katika mkutano wa baraza eneo la Likoni, Kamishna wa kaunti hiyo Nelson Marwa amesema kuwa maafisa hao wanaobugia mvinyo watafutwa kazi endapo watapatikana.

Marwa amewatahadharisha maafisa hao dhidi ya kuegesha magari ya serikali nje ya mikahawa na vilabu. 

“Tumeona mara nyingi baadhi ya maafisa wa usalama wanaegesha gari za serikali nje ya mikahawa na katika vilabu. Serikali ilianzisha kampeni ya kupigana na walanguzi na watumizi wa mihadarati pamoja na pombe haramu, mbona wewe afisaa unaenda kuegesha gari hapo na kuanza kunywa, tutakuchulia hatua,”alisema Marwa.

Kamishna huyo wa kaunti ya Mombasa amewahimiza maafisa wa usalama kuonyesha mfano bora kwa wakazi ikiwa wana malengo ya kupiga vita utumizi wa mihadarati na pombe haramu.

 Marwa amewataka viongozi wa serikali, maafisa tawala na wazee wa nyumba kumi kushirikiana na maafisa wa usalama kuwasahidia vijana kujinasua katika utumizi wa mihadarati na pia kuwasaka walanguzi wakuu.

Oparesheni ya kuwasaka walanguzi wa dawa za kulevya na pombe haramu imechangia pakubwa kupungua kuenea kwa bishara hiyo haramu.Zaidi ya vijana 95 kufikia sasa wamejisalimisha kwa viongozi wa serikali na mashirika ya kijamii ili kupata usaidizi na kujinasua katika jinamizi hilo.