Viongozi kaunti ya Nakuru wanahoji alikokuwa seneta wa kaunti hiyo James Mungai wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Rais na naibu wake walikuwa Nakuru Jumatano na Alhamisi.

Baadhi ya viongozi wametaja hatua hiyo kama “ukosefu wa heshima kwa Rais”, haswa baada ya kubainika kwamba seneta Mungai maarufu kama 'Jemo' pia hakufika kwenye mkutano wa viongozi uliokuwa kwenye Ikulu ya Nakuru.

Kati ya waliohudhuria mkutano huo ni maseneta Martha Wangari, Liza Chelule, Paul Njoroge na wabunge 10 ikiwemo Kimani Ngunjiri wa Bahati na Samwel Arama, pamoja na gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua. Mbunge wa Rongai Raymond Moi pia hakuhudhuria mikutano ya rais.

Akizungumza na mwandishi huyu kwa njia ya simu mnamo Ijumaa, seneta Wangari ambaye ni mteule alisema: “Licha ya ziara ya rais kuwa na manufaa kwa wakaazi wa kaunti hii, seneta ambaye alichaguliwa kwa kura nyingi na wakaazi kuwawakilisha, hakuonekana kwenye misururu ya mikutano hiyo.

Kwa upande wake seneta Paul Njoroge alidai “imekuwa jambo la kawaida kwa Mungai kukosa kuhudhuria mikutano muhimu ambayo huangazia mahitaji ya kaunti ya Nakuru”.

Kulingana na seneta Njoroge, hakuna anayejua aliko seneta Mungai kwani amekuwa haonekani katika kaunti hiyo tangia kuchaguliwa kwake.

Hayo yanajiri siku chache tu baada ya shirika la mzalendo Trust kuorodhesha wabunge 27 ambao hawakuzungumza bungeni mwaka wa 2015, huku mmoja akitoka Nakuru.