Maseneta pamoja na wawakilishi wadi wanatarajiwa kuandaa kongamano mjini Mombasa siku ya Jumatatu.
Kongamano hilo litakaloandaliwa katika hoteli ya kifahari ya Flamingo beach, litawaleta pamoja maseneta na wawakilishi wadi kutoka kaunti zote 47 nchini.
Mkutano huo utakuwa wa kwanza kabisa miongoni mwa viongozi hao tangu mfumo wa ugawaji wa mamlaka mashinani uanze kutumika.
Akiongea na wanahabari, mwenyekiti wa kamati ya ugawaji mamlaka na rasli mali Profesa Wilfred Leisan alisema mkutano huo sio pinzani na ule ulioandaliwa na magavana Meru.
Leisan alisema kuwa kongamano hilo linanuia kuwaleta viongozi hao kwa meza moja ili kujadili mafanikio ya mfumo wa ugatuzi.
"Kongamano hili litawaleta pamoja viongozi wanoahusika katika kuunda miswada tofauti tofauti ili kutupa nafasi ya kupiga darubini utendakazi wetu,” alisema Leisan.
Leisan alikuwa ameandamana na katibu wa chama cha wawakilishi wadi nchini Bwana Albert Kochei.