Mashabiki sita wa miamba wa soka nchini Gor Mahia almaarufu Kogallo, Jumatatu walifikishwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi na kushtakiwa kwa kuzua rabsha na hatimaye kusababisha hasara.
Siku ya Jumamosi, Gor Mahia ilinyukwa bao moja kwa nunge na Tusker FC kwenye mechi baabu kubwa ya ligi kuu ya soka nchini (KPL) iliyochezwa ugani Nyayo, hali iliyoasababisha baadhi ya mashabiki hao kutamba katika barabara ya Uhuru jijini Nairobi, na kuzua vurugu.
Sita hao watalipia gharama iliyosababishwa na wenzao ya kupiga mawe magari ya abiria, na kusababisha hasara ya shilingi alfu 73.
Sita hao Joseph Omolo, Sabastian Nduvili, Syla Aguta, James Owuor Warera, Austine Asino Owuor na Kennedy Mbola, walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani jijini Nairobi Daniel Ogembo.
Watano walikanusha mashtaka, isipokuwa James Owuor Warera aliyekiri mashtaka yote matano.
Hakimu Ogembo aliwa-achilia watano waliokanusha mashtaka kwa dhamana ya shilingi alfu 20 pesa tasilimu, huku mmoja aliyekiri mashtaka akitarajiwa kurejeshwa kortini Jumanne hii kuhukumiwa rasmi.
Mabingwa watetezi Gor Mahia ni wa tisa ligni kwa alama 11, baada ya kucheza mechi tisa msimu huu; kushinda mbili, kutoka sare tano na kupoteza mechi mbili muhimu dhidi ya watani wa jadi AFC Leopards na Tusker FC.