Afisa wa polisi akiwa nje ya Mahakama ya Shanzu hapo awali. Picha/ the-star.co.ke

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hakimu Diana Mochache wa Mahakama ya Shanzu ameitaka kesi inayowakabili washukiwa wanne wa ulanguzi wa mihadarati kuharakishwa.

Washukiwa hao, Nabil Loo Mohammed, Bakari Kali Bakari, Stephen Vicker Mangira na Lilian Bernard Martin walitiwa mbaroni Jijini Mombasa mnamo Februari 2017 katika oparesheni dhidi ya mihadharati.

Washukiwa hao pia walinaswa na shilingi milioni 18 pesa taslimu.

Mashahidi sita wanatarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya washukiwa hao mnamo Machi 22 na Aprili 13, 2017.

Kwa mujibu wa kiongozi wa mashataka, mashahidi hao watajumuisha maafisa wa usalama pamoja na raia, na huenda idadi ya mashidi ikafikia 15 uchunguzi utakapokamilika.

Akizungumza siku ya Alhamisi, Hakimu Mochache alizitaka pande husika kuharakisha uchunguzi ili kesi hiyo iweze kumalizika katika muda muafaka.

"Kulingana na Jaji mkuu kesi za dhulma dhidi ya watoto, mihadarati, uwindaji haramu na ugaidi zinapaswa kupewa kipao mbele. Nataka ikiwezekana mashahidi watatu kuwasilishwa mahakamani kwa siku ili kesi hii iamuliwe kabla ya mwaka ujao,” alisema Mochache.

Upande wa mashtaka pia ulitoa stakabadhi zitakazo wawezesha kuwasilisha risiti za benki mahakamani kama ushahidi, badala ya kutembea na hela ambazo washukiwa hao walinaswa nazo, kwa kuwa ni nyingi.

Upande huo pia ulitaka washukiwa hao kutoachiliwa kwa dhamana na kusema kuwa mshukiwa wa kwanza anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika biashara ya mihadarati na endapo atachiliwa, huenda akatatiza uchunguzi.

Aidha, walisema kuwa washukiwa wa pili na wa nne ni raia wa Tanzania na endapo watapewa dhamana, itakuwa rahisi kwao kutoka nchini, na pia huenda wakawatatiza mashahidi.

Kesi hiyo itatajwa tena Machi 16, 2017.