Jengo la mahakama ya Mombasa. Mashahidi wasema polisi walimpiga raia huyo akiwa kituo cha polisi cha Diani. [Picha: the-star.co.ke]
Mashahidi wawili katika kesi ya kuchunguza kifo cha raia wa Uingereza wameiambia mahakama kuwa maafisa wa polisi walimpiga muingereza huyo akiwa katika kituo cha polisi.
Kwa mujibu wa maelezo ya polisi, Alexender Monson alifariki Mei 19 mwaka 2012 katika hospitali hiyo baada ya kubugia dawa za kulevya, hii ikiwa ni baada ya kutiwa mbaroni na maafisa wa polisi wa kituo cha Diani akiwa na mihadarati.
Shahidi Yusufu Salim Matumizi na Abdalla Sufiani ambao walikuwa wameshikwa na kufungiwa katika kituo cha polisi cha Diani, wamesema kuwa maafisa wawili walimgungesha na chini mara mbili muingereza huyo.
Wamesema waliwaona polisi hao wakigongesha chini kichwa cha raia huyo ambaye alikuwa ametiwa mbaroni kwa madai ya kuwa na mihadharati.
Siku ya Jumanne afisa John Maina na Keneth Mutai ambao ni mashahidi katika kesi hiyo, waliambia mahakama kuwa muengereza huyo alipoteza fahamu akiwa katika kituo hicho cha polisi,hali iliyowafanya kumkimbiza katika hospitali ya Diani Palm Beach, ambako aliaga dunia.
Siku ya Jumatatu afisa mwengine Isaa Saidi aliambia mahakama kuwa muingereza huyo alifariki akiwa amefungwa pingu mkononi akiwa hospitalini.
Kwa sasa mashaidi 28 wametoa ushahidi wao kuhusiana na kifo hicho,huku wengine zaidi ya 20 wakitarajiwa kutoa ushahidi wao.
Kesi hiyo itaendelea 6,10,2017,ambapo mashahidi wengine watatoa ushahidi wao.