Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar akitoa ushahidi wake mahakamani siku ya Jumatatu. [Picha/ standardmedia.co.ke]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar amepata pigo baada ya mashahidi wake saba kuondolewa katika kesi ya kupinga ushindi wa Gavana Hassan Joho.Mashahidi hao saba ni kati ya 19 ambao walikuwa tegemeo kuu la Omar kwenye kesi hiyo.Haya yanajiri baada ya mawakili wa Joho, wakiongozwa na Denis Mosota, kutaka mashahidi hao kutoshiriki kwenye kesi hiyo kwa madai kuwa ushahidi wao sio wa ukweli.“Ushahidi wa mashahidi wa Omar sio wa ukweli kwani umejaa uvumi. Mashahidi hao hawafai kushiriki kwenye kesi hii,” alisema Mosota.Akitoa uamuzi wake siku ya Alhamisi, Jaji Lydia Achode alisema kuwa mahakama haitazingatia ushahidi ambao haumbatani na kanuni za sheria za uchaguzi kwa mujibu wa katiba, na kuagiza mashahidi hao kuondolewa kwenye kesi hiyo.“Mahakama haitazingatia ushahidi wowote wa uvumi ambao si wa ukweli. Mahakama itafuata haki na usawa kwa mujibu wa katiba,” alisema Achode.Jaji Achode aidha alisema kuwa hatazingatia nakala za fomu za matokeo zilizowasilishwa mahakamani na Omar ambazo hazina muhuri wa Tume ya IEBC.Mosota na Mohammed Balala ambaye pia ni wakili wa Joho waliwasilisha ombi la kutaka kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo kwa kusema kuwa nakala zilizowasilishwa hazina muhuri wa IEBC.Jaji Achode alitupilia mbali ombi hilo na kusema kuwa kesi hiyo itaendelea.Hata hivyo, alionya kuwa hatazingatia ushahidi wowote wa uvumi utakao wasilishwa mbele yake.Omar alitoa ushahidi wake katika kesi hiyo siku ya Jumatatu.Omar alisema kuwa kulikuwa na udanganyifu mwingi wa kura katika vituo mbali mbali Kaunti ya Mombasa, na kutoa mfano wa wapiga kura waliopewa zaidi ya makaratasi mawili ya kupigia kura katika eneo bunge la Changamwe.Aidha, Omar alisema kuwa wapiga kura wengi walifurushwa baada ya majina yao kukosekana kwenye vifaa vya Kiems.“Wapiga kura walifurushwa katika vituo vya kura baada ya majina yao kukosekana kwenye vifaa vya Kiems, hatua ambayo ni ukiukaji wa haki za wapiga kura,” alisema Omar.Omar ameitaka mahakama kutupilia mbali ushindi wa Joho na uchaguzi huo kufanyika upya.