Wafanyabiashara katika soko kuu la Kongowea wamelalamikia uwepo wa mashimo yaliyo sheheni uvundo katika soko hilo jambo ambalo linawakosesha wateja hasa wakati huu ambapo biashara imenoga kutokana na sherehe za Pasaka.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mashimo hayo ambayo huzuia maji chafu hutoa harufu mbaya kwa wateja jambo ambalo limewafanya wengi wa wateja kuepuka kufika sehemu hizo.

Wafanyabiashara hao kupitia kwa msemaji  wao Robert Mlai, wamesema kuwa imekuwa hatari wakati magari ya mizigo yanapoingia sokoni humo kutokana na mashimo hayo.

Mlai aliongeza kwa kusema kuwa wanalazimika kukaa kando ya biashara zao kwa kuhofia kuangukiwa na magari na hata harufu mbaya inayotokana wakati mashimo hayo yanachubuliwa.

Mlai pia amesema kuwa wateja wamekuwa wakikwepa sehemu hizo kwa kuhofia maradhi yanayoambatana na mazingira mabaya na hata pia kuhofia usalama wao.

Aidha, Robert amewataka viongozi washughulikie suala hili la mashimo na kuongeza kuwa ni jambo la aibu endapo watalii watafika na kuona hali mbaya ya soko hilo.