Share news tips with us here at Hivisasa

Wadau wa utalii wamesema utalii umeimarika kusini mwa Pwani wakati huu ambapo mashindano ya boti yanapoendelea katika eneo hilo, ikilinganishwa na msimu kama huu mwaka jana.

Mashindano hayo ya boti ambayo ni ya kipekee Afrika Mashariki, huwashirikisha wavuvi, makundi mbalimbali ya kitamaduni pamoja na wafanyibiashara ambapo lengo kuu ni kuwaunganisha na kujitangaza kitalii.

Akiongea wakati wa mashindano hayo siku ya Jumapili, Mkuu wa Idara ya Utalii katika Kaunti ya Kwale Adhan Mukhtar, alisema kuwa wamefurahishwa na idadi kubwa ya watalii waliozuru eneo hilo la Pwani.

“Watalii wamekuja kwa wingi na wanakula wakijivinjari huku wakifurahia kutazama mashindano ya boti. Hii ni njia moja ya kuunganisha wavuvi wetu pamoja na makundi ya kitamaduni,” alisema Mukhtar.

Kwa upande wao, wavuvi walioshiriki mashindano hayo walielezea furaha yao huku wakionyesha matumaini katika siku zijazo.

“Mwaka jana tulikuwa hapa lakini tukashindwa na tukaibuka nambari tano. Mwaka huu tumejitahidi tukashinda na mbali na hivyo, mashindano haya pia yametupatia fursa kubwa sana,” alisema Majaliwa, mmoj a wa wavuvi hao.

Sekta ya utalii katika ukanda wa Pwani imeanza kuinuka huku wadau katika sekta hiyo wakitumia mashindano pamoja na hafla mbalimbali kujaribu kutangaza biashara hiyo kimataifa.

Kusini mwa Pwani ni moja kati ya maeneo yenye vivutio vikubwa vya utalii ikiwa ni pamoja na fuo za bahari.

Mapema mwaka jana, ufuo wa Bahari wa Diani ulioko eneo hilo ulitajwa kwenye orodha ya fuo bora za bahari barani Afrika.