Mashirika ya kijamii nchini yamemtaka Gavana wa Kilifi Amason Kingi kujiuzulu ili kutoa nafasi kwa Tume ya EACC kufanya uchunguzi kuhusiana na sakata la kupotea kwa takribani shillingi millioni 52.
Akizungumza kwenye kongamano la mashirika hayo jijini Nairobi siku ya Jumapili, afisa mkuu wa mashirika hayo Morris Odhiambo, alisema Gavana Kingi anapaswa kuondoka mamlakani ili kupisha maafisa wanaoendesha uchunguzi huo.
Odhiambo alisema kuwa uchunguzi huo huenda ukachukua muda mrefu kukamilika iwapo Kingi na maafisa wake watasalia kuwa mamlakani.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba viongozi wa Kaunti ya Kilifi wanahusika katika sakata hilo la mamilioni ya fedha ilihali ripoti zinaonyesha kuwa wakaazi wanakumbwa na baa la njaa linalowalazimu kutumia matunda mwitu kama chakula chao cha kila siku.
Aliitaja hatua hiyo ya kupotea kwa mamilioni ya fedha kama aibu, na kuwakosoa viongozi wa kaunti hiyo kwa kile alichokitaja kama kutokuwa na huruma kwa wananchi waliowaweka mamlakani.
Mwanaharakati huyo aidha alisema kuwa japo tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imeanzisha uchunguzi, ni sharti afisi ya mkaguzi mkuu wa serikali kutoa taarifa kamili kuhusiana na sakata hilo.
Alisisitiza kuwa ni sharti adhabu kali kuchukuliwa kwa yeyote atakayepatika kuhusika kwenye wizi huo wa fedha za umma.