Mashirika mbalimbali ya kijamii nchini yanaendelea kushinikiza kuidhinishwa kwa mswada wa usawa wa jinsia ili kuhakikisha kuwa miswada inayowasilishwa bungeni inapata uungwaji mkono.
Wakiongozwa na afisa wa haki na sheria katika Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Afrika Francis Gamba, wanaharakati hao wamesema kuwa watahakikisha kuwa wametumia hatua za kisheria kuhakikisha kuwa mswada huo unarejeshwa bungeni na kupitishwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Gamba alisema kuwa muungano wa mashirika ya kijamii uko tayari kuelekea mahakamani kuhakikisha kuwa bunge linashinikizwa kupitisha mswada huo wakati utakaporejeshwa tena bungeni.
Gamba alisema kuwa hatua ya bunge kutopitisha mswada huo bungeni wiki iliyopita imeonyesha wazi kuwa bunge la kitaifa halijazingatia uwajibikaji pamoja na utekelezaji wa Katiba.
"Tumeona kuwa bunge limeshindwa kupigania haki za Wakenya wanyonge na kwa sababu hiyo, sisi tuko tayari kutumia sheria hata kama ni kwenda mahakamani ili mswada huu upitishwe bungeni,” alisema Gamba.
Mashirika hayo sasa yanapanga kuzuru mashinani kuwahamasisha wakaazi pamoja na viongozi wa kisiasa kutambua umuhimu wa mswada huo wa usawa wa jinsia.