Hatua ya Kenya kutaka kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kule mjini Hague imepingwa vikali na baadhi ya Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na yale ya kijamii humu nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mashirika hayo yakiongozwa na lile la Haki Afrika, yamesema kuwa hatua hiyo huenda ikachangia hata viongozi wengine kutekeleza maovu zaidi kwani watakuwa na mamlaka zaidi kutokana na Kenya kujiondoa kwenye mkataba huo wa Roma.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano kwenye kongamano la Muungano wa Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, Afisa wa Haki na Sheria katika Shirika la Haki Afrika Francis Auma Gamba, amesema kuwa kama Muungano wa Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nchini hawatakubali Kenya kujiondoa kwenye mkataba huo wa Roma kwani itapeyana nguvu kwa mataifa mengine Afrika kujiondoa.

Amesema kuwa watakafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa wanapata uungwaji mkono na Wakenya pamoja na mashirika mengine ya haki za kibinadamu katika nchi za Afrika Mashariki na hata Baraza zima la Afrika ili kuzuia Kenya kujiondoa kwenye mkataba huo.

"Kama Muungano wa Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu,  kamwe hatutakubali Kenya kujiondoa kwenye mkataba wa Roma kwa sababu Mahakama hiyo ya ICC imewafanya viongozi wengi kuhofia kuwadhuluma wananchi," alisema Auma.

Hatua ya Kenya kutangaza kujiondoa katika Mahakama hiyo ya ICC iliyoundwa na Mataifa ya Afrika na kubuni mkataba wa Roma imejiri baada ya Wakenya sita waliyokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Wakenya zaidi ya 1000 kesi yao kutupiliwa mbali.