Tofauti na dhana ya wengi, sio mashirika yote yasiyo ya kiserikali (NGO) yanayoanzishwa na wale walio na fedha.
Hilo limekaririwa na Tina Achieng, mwanachama kutoka kwa shirika la kimataifa la Scopus Haddassah International Kenya ambalo linajihusisha na maswala ya mtoto wa kike na maswala ya watu walio na matatizo ya kiakili miongoni mwa mengine.
Achieng, kwenye mahojiano na wanahabari mjini Nakuru amesema dhana hiyo imepelekea wengi na haswaa walio na ulemavu kupuuza mikutano yao wanayolenga kuwafanyia mazoezi walio na matatizo ya uti wa mgongo (physiotherapy) na haswaa baada yao kuarifiwa kuwa hawatapewa nauli.
Dhana hii, kwa muujibu wake, imepelekea wengi kukosa kuwapa ufadhili kwani kulingana nao, mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kawaida huwa ana fedha nyingi.
"Kuna changamoto nyingi ambazo tunakumbana nazo kwani kama shirika lisilokuwa la kiserikali wengi hudhania kuwa tuna fedha nyingi. Hata wale walio na ulamavu hukosa kuhudhuria baadhi ya hafla zetu tunazolenga kuwafanyia mazoezi ya uti wa mgongo wanaposikia kwamba hatuwapi nauli ya kuwafikisha kwenye hafla hizo," alisema Achieng.
Wakati huo huo, amesema kwamba licha ya uwepo ya siku ya qwalemavu ambayo imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka mingi hapa nchini, baadhi ya walio na ulemavu wangali wanakumbana na unyanyapaa (stigma) kwanibaadhi ya watu wangali hawajawakubali kwenye jamii.
Ni hatua ambayo anasema imepelekea baadhi ya watu kuwafungia walio na ulemavu kwenye nyumba zao na pia kuwaficha kwani hawawachukulii watu hawa kama walio na manufaa kwenye Jamii au watu ambao wanaweza kuwafaa katika siku za usoni.
Hivyo basi, amewahimiza wakenya kuwaonyesha upendo walio na ulamavu na pia kutowabagua.
"Kuna hali ya unyanyapaa kwenye Jamii ambayo ingali inawakumba walio na ulemavu. Isitoshe, katika Jamii hatuwakubali walio na ulamavu na haswaa watoto walio na ulemavu. Hatuwaschukulii kama watu ambao wanaweza kutusaidia katika siku za usoni. Watu wengi wanawafungia watoto hao makwao na kutokana na hilo, hii leo tunawahimiza wakenya kutowafungia Watoto au tu yeyote aliye na ulemavu. Tunawahimiza wakenya kuwapenda na pia kuwajali walio na ulemavu," aliongeza Achieng.
Ni usemi ambao amekariri huku dunia nzima ikiadhimisha siku ya kimataifa ya walio na ulemavu tarehe 3 Desemba mwaka huu.