Kipande cha ardhi ya kibinafsi chenye ekari 8.3 kinachomilikiwa na familia ya Muhidin katika eneo la Kongowea Maweni, Kaunti ya Mombasa, kinaendelea kuwatia tumbo joto wakaazi kutokana na uamuzi wa mahakama wa kulipa deni la ada ya shilingi milioni 35.
Mwenyekiti wa Tume ya Ardhi nchini Mohammad Swazuri alisema kuwa wakaazi hao walivamia shamba hilo na kuanza kuishi humo tangu mwaka wa 1993.
Akizungumza siku ya Jumamosi mjini Mombasa, Swazuri alisema kuwa wakaazi hao wamekubaliana kulipa ada hiyo ili kufidia deni hilo lililotokana na wao kuishi kwenye ardhi hiyo kinyume cha sheria.
Aidha, aliongeza kuwa serikali inafanya kila juhudi kutatua mizozo ya ardhi katika eneo hilo.
“Migogoro yote lazima yatatuliwe kwa kufuata sheria. Tusipofanya hivyo, basi muafaka huatapatikana,” alisema Swazuri.
Mwenyekiti huyo aidha amewataka wakaazi hao kushirikiana na serekali kuu pamoja na ile ya kaunti ili swala hilo liweze kutatuliwa.