Maskwota wanaoishi katika kipande cha ardhi cha Matopeni, eneo bunge la Nyali, wamepinga hatua ya Tume ya ardhi NLC, kutaka kuwaondoa katika ardhi hiyo.
Wakaazi hao wanaodai kuishi katika ardhi hiyo kwa miaka mingi wamepinga barua iliyotumwa na NLC kuonyesha kwamba sehemu hiyo inamilikiwa na mtu binafsi.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja baina ya wakaazi na viongozi wa mashirika mbalimbali, mzee wa kijiji hicho cha Matopeni Julius Kanampiu, alisema hawakubaliani na barua hiyo.
“Hatua ya kutuondoa haijafuata sheria. Mara kwa mara tumekuwa tukitishiwa na barua za kutaka tuondoke lakini hii ya sasa imezidi na hatutoki,” alisema Kanampiu.
Wakaazi hao wamesema walipokea barua kutoka kwa tume ya NLC ikiwataka kuondoka kwa madai kwamba kuna mtu binafsi aliyenunua kipande hicho.
Barua hiyo imemtaja mnunuzi wa shamba hilo kama Omar Awadh.
Aidha, wakaazi hao wanamlaumu mwenyekiti wa tume hiyo Mohamed Swazuri kwa madai kuwa anatumiwa na baadhi ya mabwanyenye kuwanyanyasa wananchi.
Walisema kuwa licha ya Swazuri kuwa mzaliwa na mkaazi wa Pwani, bado hawajaona faida yake licha ya dhulma wanazopitia kila siku huku swala la ardhi likisalia kuwa tata eneo hilo.
“Tunamtaka Swazuri aje mwenyewe hapa tuzungumze tutafute suluhu na sio kutuma barua tu,” alisema mkaazi mwingine.
Barua hiyo iliyotumwa tarehe 23 mwezi Juni kutoka kwa Tume ya ardhi inaagiza maskwota hao kuondoka katika kipande hicho cha ardhi chenye ukubwa wa zaidi ya ekari tatu.
Wakati huo huo, Kanampiu amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha kwamba wanapata hati miliki za ardhi.
“Tunajua rais anakuja Mombasa mwezi wa nane na tunaomba achukue fursa hiyo kututembelea na kutupatia hati miliki ili tuache kusumbuliwa,” alisema Kanampiu.