Maskwota katika ukanda wa Pwani wamepongeza hatua ya Waziri wa Ardhi Jacob Kameinyi kutaka kuongezewa pesa zaidi ili kurahisha zoezi la kutoa hati miliki.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumanne, wakaazi hao walisema kuwa wanaishi kwa hofu kwani hawana vibali vya kuonyesha kumiliki ardhi kisheria.
Wakiongozwa na Saudina Kimani, wakaazi hao wa Likoni, walisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa wizara hiyo kutimiza malengo yake.
Kauli hii inajiri baada ya wizara ya ardhi kusema kuwa inataka bajeti yake iongezwe kwa shilingi bilioni mbili zaidi, ili kuiwezesha kutoa hati milioni moja za umiliki wa ardhi kabla ya mwisho wa mwaka ujao.
Waziri wa Ardhi, Profesa Jacob Kaimenyi, alisema wizara hiyo imetoa zaidi ya hati milioni tatu za umiliki ardhi kwa Wakenya tangu mwaka wa 2013.
Hata hivyo, waziri huyo alisema fedha ambazo wizara hiyo inazo kwa sasa haziwezi kutosha kugharamia zoezi la kutoa hatimiliki zaidi.
Akizungumza jijini Nairobi siku ya Jumanne, Kaimenyi alisema makundi nane yamebuniwa kusimamia na kuharakisha utoaji wa hatimiliki kwa maskwota katika maeneo ambako ardhi haijagawanywa.
Aidha, Kaimenyi alisema wizara hiyo itazindua zoezi la kuweka mipaka ya ardhi ili kuzuia kuwepo kwa ksei zinazotokana na mizozo ya umiliki ardhi kwa kutumia mfumo wa gharama nafuu.