Masomo katika Shule ya msingi ya Maji Safi, Likoni, yalitatizika kwa muda baada ya kamati ya shule hiyo kudai kuwa mwalimu mkuu alikuwa akifuja fedha za maendeleo.
Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Bwana Said Ibrahim, alidai kuwa mwalimu huyo amefuja kitita cha shilingi laki mbili unusu za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa na vyoo, pamoja na ununuzi wa dawati.
“Tutaongoza maandamano kupinga ubadhirifu huo wa pesa za shule iwapo mwalimu huyo hatapewa uhamisho,” alisema Bwana Ibrahim.
Ibrahim alisema kuwa walipomuuliza mwalimu huyo pesa za maendeleo zilipo, alisema kuwa hana pesa zozote, huku ikikadiriwa kuwa shilingi 250,000 kati ya shilingi 472,000 zilizokuwa zimekusanywa katika muhula wa kwanza, zilikuwa zimefujwa.
"Madai haya si ya kweli. Mimi huwa sihusiki na pesa kwa vile shule ina mhasibu anayeshughulikia maswala hayo,” alisema Bwana Henry Nanga, kama alivyonukuliwa na Baraka FM.
Aidha, inadaiwa kuwa walimu katika shule hiyo wamegoma kufuatia kutolipwa mshahara wa miezi mitatu.
Wahasibu kutoka kwa idara ya elimu tayari wameanza uchunguzi kuhusu kisa hicho.