Matarajio ya baadhi ya wenyeji kutoka eneo la Changamwe kuhutubiwa na Waziri wa Ardhi Jacob Kaimenyi kwenye hafla ya uzinduzi wa ruwaza ya 2035 ya Kaunti ya Mombasa iliambulia patupu baada ya waziri huyo kukosa kuhudhuria hafla hiyo.
Waziri kaimenyi ambaye alikuwa miongoni mwa wageni alikwa, alikosa kwenye hafla kwa madai ya kuhofia makali ya mzozo wa kutolewa kwa makataa ya kuhamishwa kwa wenyeji walio na makazi karibu na Uwanja wa ndege wa Moi.
Agizo hilo limeshuhudia makabiliano ya maneno baina ya mshrikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa na baadhi ya wawakilishi wa wadi wa maeneo husika.
Wakaazi ambao walihudhuria hafla hiyo, wakiongozwa na mzee Mwinyi Ngao walisema kuwa walitarajia waziri huyo kuhudhuria mkutano huo ili kuangazia suala hilo na kutoa mwelekeo wa sawa, badala ya kuendelea kushuhudia majibishano baina na maafisa wa serikali.
Mzee huyo pamoja na waathiriwa wenzake wametoa wito kwa serikali kuu kutafuta suluhu mwafaka baina yao ili kuwapa matumaini wakazi hao ambao kwa sasa wameathirika kimawazo.
Waziri Kaimenyi aliwakilishwa na katibu kutoka Wizara ya Ardhi Mariamu El Maawy ambaye alisoma hotuba kwa niaba ya waziri huyo.