Bodi simamizi zinazoingisha siasa za ukabila kwenye usimamizi wa shule zimeonywa vikali.
Akihutubu kwenye mkutano uliowaleta pamoja walimu wakuu wa shule za upili kutoka eneo la Gusii kwenye shule ya upili ya wavulana ya Kisii siku ya Jumatano, waziri wa elimu Fred Matiang'i alisema bodi za aina hiyo zitavunjiliwa mbali.
"Kuna baadhi ya wanachama wa bodi za shule wanaoingisha siasa za ukabila kwenye usimamizi wa shule ila wacha wafahamu kwamba kamwe serikali haitowavumilia," alisema Matiang'i.
Matiang'i aidha aliongeza kwa kuonya vikali walimu wakuu wa shule dhidi ya kuwaruhusu walimu kutohudhuria shule kwa sababu zisizoeleweka hali inayoathiri viwango vya elimu nchini.
"Walimu wengi hukosa kuhudhuria vipindi darasani kutokana na hali ya kuruhisiwa na walimu wakuu kutohudhuria shule kwasababu zisizo mwafaka na mimi waziri nitahakikisha kuwa tabia hiyo hairuhusiwi," aliongezea Matiang'i.