Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i ameitaka bodi ya elimu nchini kutambua dini ya Kiislamu na kuwapa wanafunzi Waislamu nafasi ya kuswali wakati wa shule.
Matiang'i amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kukomesha visa vya udhalilishaji wa kidini wanavyopitia wanafunzi wa dini ya Kiislamu wanaosomoa shule mbalimbali nchini zisizo za Kiislamu.
Akizungumza katika mkutano wa walimu wa shule za upili mjini Mombasa, Matiang'i alisema kuwa amepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa Kiislamu kwamba wamekuwa wakishurutishwa kuhudhuria misa za kanisa na kutovaa hijab.
“Hili suala la kuwabagua wanafunzi kwa msingi wa kidini sharti likome. Lazima tutambue na tuziheshimu dini na imani za wengine katika jamii pahali popote pale,” alisema Matiang'i.