Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang'i, amepiga marufuku ziara za wazazi za kuwatembelea wanao shuleni pamoja na mapumziko ya muda wakati wa masomo ya muhula wa tatu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye kikao na waandishi wa habari mjini Nairobi siku ya Jumatano, Matiang'i alisema kuwa amechukua hatua hiyo ili kuzuia visa vya wizi wa mtihani.

Waziri huyo alisema kuwa wanafunzi pia hawatakuwa na likizo fupi ya kati kati ya muhula wa tatu, kwa kuwa muhula huo mara nyingi huwa mfupi ikilinganishwa na mihula mingine.

Aidha, Matiang'i alisema kuwa wizara yake imerefusha muhula wa pili kwa muda wa wiki moja, ili kuwapa walimu nafasi ya kukamilisha mtaala.

Alisema kuwa muhula wa pili uliotarajiwa kuisha Agosti 5 utamalizika Agosti 12, 2016.

Vile vile, waziri huyo alitangaza kuwa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE wa mwaka huu utaanza mnamo Novemba 7 hadi tarehe 30, huku wa KCPE ukiratibiwa kufanyika kati ya Novemba 1 na 3, 2016.