Wizara ya Elimu nchini imepuzilia mbali maadai ya muungano wa walimu wa Knut kuwa hawakuhusishwa katika kujadili sheria za mfumo mpya wa elimu zilizotangazwa na wizara hiyo.
Akizungumza mjini Mombasa baada ya kukutana na waalimu 105 kutoka shule za upili za kitaifa nchini siku ya Jumanne, Waziri Fred Matiang'i alisema kuwa sheria zilizopitishwa hapo awali ndizo zitatumika.
Aidha, alisema kuwa maagizo ya kufanikisha sheria hizo zishatumwa katika afisi za maafisa wa elimu katika kaunti zote.
Waziri huyo pia alisema kuwa aliwashirikisha washika dau wote katika sekta ya elimu kabla ya kufanya mabadiliko hayo.
“Sikuvunja sheria yoyote kama inavyodaiwa na katibu mkuu wa muungano wa walimu Wilson Sossion kwa vile niliwashirikisha wadau wote kabla ya kufanya mabadiliko hayo,”alisema Matiang'i .
Bwana Sossion amekuwa akimkashifu Waziri Matiang'i kwa kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu, kwa kusema kuwa mfumo huo mpya haukuwa unafaa.