Waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i ametishia kuwasimamisha kazi walimu ambao wako wakurugenzi katika viwanda vya majani chai kwani wameacha sekta ya elimu na kujihusisha na masuala mengine tofauti.
Kulingana na Matiang’I, walimu ambao ni wakurugenzi hutumia mda wao mwingi katika masuala ambayo si ya elimu, jambo ambalo limerudisha nyuma viwango vya elimu.
Akizungumza siku ya Jumapili katika shule ya upili ya Nyambaria iliyoko eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira wakati wa kuwazawadi wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa kidato cha nne mwaka jana, waziri Matiangi aliwataka walimu hao ambao hufanya kazi tofauti kando na ile ya ualimu kuacha kazi au awafute kazi mara moja.
“Viwango vya elimu vimedorora katika shule zetu kufuatia walimu wengi hufanya kazi ingine tofauti kando na masomo. Baadhi ya walimu ni wakurugenzi katika viwanda vya majani chai na hutumia mda wao mwingi katika ukurugenzi kando na masomo,” alisema Matiang’i.
“Nawaomba walimu hao ambao wanafanya kazi hiyo waache kazi mara moja au nitawasimamisha kazi maana tunahitaji viwango vya elimu kuinuka zaidi katika shule zetu,” aliongeza Matiang’i.