Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i amewakosoa viongozi wanaotumia wanafunzi kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Matiang'i amesema kwamba tabia hiyo inapaswa kusitishwa mara moja.
Aidha, Waziri huyo ameunga mkono hatua ya mshirikishi mkuu wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa ya kuwazuia wanasiasa kusambaza chakula cha mchana kwa wanafunzi wa darasa la nane waliokuwa wakifanya mtihani wao wa kitaifa wa KCPE.
Matiang’i alihoji kwamba wanasiasa hawapaswi kuhitilafiana na ratba ya elimu nchini.
Akitoa kauli hiyo huko Pwani kusini, Matiang’i alisema wanasiasa hawapaswi kuzuru shule mbalimbali wakati wa mitihani ya kitaifa na kusambaza vyakula vilivyo na majina na picha zao.
Aliitaja tabia hiyo kama isiyolenga kuimarisha hadhi ya masomo kwa wanafunzi.
“Kubandika picha katika nakala za mitihani ya kitaifa kamwe haina lengo la kuimarisha viwango vya elimu bali inawapotosha wanafunzi na ni lazima mtindo huo usitishwe,” alisema Matiang’i.
Alisema kwamba swala hilo la kusambaza vyakula vya bure wakati wa mitihani ya kitaifa halitaruhusiwa sio tu mwaka huu bali hata miaka ijayo.
Matiang'i alisisitiza kuwa mwanasiasa atakayekiuka amri hiyo atakabiliwa kisheria.